9 Aprili 2025 - 21:20
Source: IQNA
Unafiki wa nchi za Magharibi katika kutetea uchomaji wa Qur’ani

Tendo la kutusi na kudhalilisha nakala za Qur’ani Tukufu katika mataifa ya Magharibi kwa kisingizio cha kulinda uhuru wa kujieleza limekuwa likirudiwa mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.

Hali hii inatokea huku ukosoaji wowote wa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina ukikabiliwa na mashinikizo makubwa na ukandamizaji katika nchi hizo hizo za Magharibi.

Kwa mujibu wa makala iliyoandikwa na Najla Mahfouz na kuchapishwa na Al Jazeera, viwango hivi viwili vya maamuzi vinadhihirisha unafiki wa wazi wa mataifa ya Magharibi kuhusu masuala ya haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.

Dondoo kutoka katika makala hiyo zinasema hivi:

Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na matukio mengi ya  kuvunjiwa heshima na kudhalilishwa kwa Qur’ani Tukufu katika nchi za Magharibi, huku wanasiasa wa mataifa hayo wakiyashabikia, kuyatetea na kuyasifia kwa kutumia kaulimbiu ya "uhuru wa kujieleza".

Wanasiasa hawa ni wale wale ambao, wanapokutana na jambo lolote wanaloona kama chuki dhidi ya Wayahudi (antisemitism), huibua kelele kubwa ambazo husikika duniani kote.

Vyombo vya habari vya Magharibi hushabikia kila mara nakala ya Qur’ani inapochomwa moto au Mtume Muhammad (SAW) anapotukanwa na badala ya kulaani wanaodhalilisha imani takatifu za Waislamu, wao huwageukia Waislamu walioghadhibika kwa uovu huo, na kuwatangaza kuwa maadui wa uhuru!

Tunauliza: Kwa nini lawama zote hizi dhidi ya Uislamu? Nani amewalazimisha waingie katika dini ya Kiislamu? Waislamu hawatawali dunia hii, hawajakandamiza haki za watu wengine, wala hawajakalia kwa mabavu nchi za watu.

Kudhalilisha imani za Waislamu hakukomei katika kuchoma moto nakala za Qur’ani pekee.

Mwaka 2012, filamu ya matusi iitwayo “Innocence of Muslims” ilitolewa hadharani. Kisha jarida la Kifaransa Charlie Hebdo likachapisha vibonzo vilivyomkashifu Mtume Mtukufu (SAW), jambo lililosababisha maandamano makubwa kutoka kwa Waislamu duniani kote.

Magharibi iliizuia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kulaani matukio hayo ya udhalilishaji, wakati huo huo watu wengi waliokosoa mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza walikumbwa na vitisho na mateso kutoka kwa vyombo vya usalama vya mataifa hayo hayo ya Magharibi.

Serikali ya Sweden  au Uswidi kwa mafano haijawahi kuruhusu kuchomwa kwa Taurati, lakini imewaruhusu wenye chuki dhidi ya Uislamu kuchoma nakala za Qur’ani mara kadhaa hadharani.

Kuchoma vitabu vitakatifu vya dini hakufanikishi lolote, wala hakupunguzi idadi ya wafuasi wake. Kinachojulikana kwa uhakika ni kwamba vitendo hivi huchochea ghadhabu na huzuni kubwa miongoni mwa waumini.

Kwa hakika, vitendo kama hivi huweza kuwachochea wengine kutaka kujifunza kilichoandikwa ndani ya vitabu hivi vya mbinguni, na hatimaye kuondoa taswira potofu waliyonayo kuhusu Uislamu na Waislamu — jambo ambalo tayari linaendelea kutokea.

Ni wazi kuwa wale wenye ustaarabu, ubinadamu na maendeleo ya kiakili, huheshimu zaidi imani za wengine, hukwepa kukashifu alama za dini, na huepuka kubeza au kudhalilisha itikadi za watu wengine — iwe kwa njia ya moja kwa moja au ya kificho.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha